Mchango wa Tamasha za Muziki Katika Ufundishaji wa Uainishaji wa Nyimbo Katika Shule za Upili Nchini Kenya

  • Emilly Angushi Magambo Kibabii University
  • Fred Wanjala Simiyu, PhD Kibabii University
  • Deborah Nanyama Amukowa, PhD
Sambaza Makala:

Ikisiri

Utafiti huu ulichunguza mchango wa tamasha za muziki katika ufundishaji na uainishaji wa nyimbo katika shule za upili nchini Kenya. Utafiti huu hasa ulilenga kupambanua uainishaji wa nyimbo katika tamasha za muziki, kudhihirisha namna uainishaji huu unavyoweza kutumiwa kufundishia uainishaji wa nyimbo darasani na kuonesha namna ambavyo uainishaji wa nyimbo katika tamasha za muziki huzisaidia nyimbo husika kutekeleza wajibu wake. Tafiti nyingi zimefanywa kuhusu ufundishaji wa fasihi simulizi lakini kuna haja ya kuchunguza njia mbadala za ufundishaji wa kipera cha nyimbo kwa sababu ni kipana mno na hata uainishaji wake unakanganya. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya utanzu inayoonesha utaratibu wa kuainisha fasihi katika misingi ya aina mbalimbali kwa kuegemea miundo na maumbo, pamoja na nadharia ya ujifunzaji kijamii ambayo inashikilia kuwa ujifunzaji ni mchakato wa utambuzi ambao hujitokeza katika muktadha wa kijamii. Sampuli iliyolengwa katika utafiti huu ilijumuisha shule zilizoshiriki katika mashindano ya tamasha za muziki ya Kanda la Magharibi. Utafiti huu ulifanywa kwenye mashindano ya tamasha za muziki kiwango cha kikanda eneo la Magharibi yaliyofanyika katika shule ya upili ya wavulana ya Chavakali iliyo katika Kaunti ya Vihiga nchini Kenya. Kauli mbiu yake ilikuwa kuboresha umoja wa kitaifa kwa kuunganisha na kuleta watu pamoja. Watafitiwa ishirini na tano walihojiwa. Mbinu ya kuteua sampuli ilikuwa ya kinasibu na ya kimakusudi. Mtafiti alitumia utazamaji na mahojiano kama mbinu za kukusanya data. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kutumia maelezo ya kiufafanuzi na kuwasilishwa kwa maandishi yaliyoambatana na mifano na picha. Mtafiti alipata kwamba nyimbo zimeainishwa katika madaraja mbalimbali kutegemea vigezo kama vile umri, mahali na maudhui. Utafiti huu ulibaini kuwa, tamasha za muziki zinaweza kuwa njia mbadala ya kufundishia uainishaji wa kipera cha nyimbo katika fasihi simulizi darasani. Umuhimu wa utafiti huu ni kuwa matokeo yake yataweza kuwafaidi wanafunzi na walimu katika ufundishaji wa nyimbo kama kipera cha fasihi simulizi.

Upakuaji

Bado hatuna takwimu za upakuaji.
Tarehe ya Uchapishaji
23 Agosti, 2019
Jinsi ya Kunukuu
Magambo, E., Simiyu, F., & Amukowa, D. (2019). Mchango wa Tamasha za Muziki Katika Ufundishaji wa Uainishaji wa Nyimbo Katika Shule za Upili Nchini Kenya. Jarida La Afrika Mashariki La Masomo Ya Kiswahili, 1(1), 35-41. Retrieved from https://journals.eanso.org/index.php/eajss/article/view/23

Makala zilizo somwa zaidi kama hii.