Tamathali za Semi Zinazosawiri Ubabedume Katika Majigambo ya Miviga ya Shilembe na Mchezasili wa Mayo ya Waisukha, Nchini Kenya kwa Mtazamo wa Semantiki

  • Mary Lukamika Kibigo Masinde Muliro University of Science and Technology
  • Susan Chebet Choge, PhD Masinde Muliro University of Science and Technology
  • Fred Wanjala Simiyu, PhD Kibabii University
Sambaza Makala:

Ikisiri

Makala hii imewasilisha baadhi ya matokeo ya utafiti wa Uzamifu uliotafitia ubabedume katika majigambo ya miviga ya Shilembe na mchezasili wa Mayo katika jamii ya Waisukha nchini Kenya kwa mtazamo wa semantiki. Utafiti huu ulihakiki tamathali mbalimbali za semi ambazo ni chuku, jazanda na majazi miongoni mwa nyingine kwa kutumia mtazamo wa kisemantiki ili kudhihirisha namna zinavyosawiri ubabedume katika miviga ya Shilembe na Mchezasili wa Mayo. Utafiti huu ulifanyika katika Kaunti Ndogo ya Shinyalu, Kaunti ya Kakamega, nchini Kenya. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili, ya kwanza ni nadharia ya Uwezo-Uume iliyoasisiwa na Robert Bly na kuendelezwa na Izugbara. Inahusu mahusiano ya wanaume na wanawake katika jamii. Nadharia ya pili iliyotumiwa ni ile ya Uchanganuzi Makinifu wa Diskosi (UCHAMAWADI). Nadharia hii ina misingi yake katika kazi mbalimbali za wataalam tofauti ulimwenguni. Nadharia mbili zilitumiwa ili kuoanisha taaluma ya Fasihi na Isimu. Utafiti huu ulitumia majigambo kumi na sita kwa kutumia uchunzaji-shiriki, dodoso, unasaji sauti na ujazaji wa hojaji. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa lugha ya majigambo inayoghaniwa na fanani hubeba tamathali za semi zinazosawiri ubabedume. Hivyo, sherehe hizi zitumiwe kama jukwaa la kuelimisha vizazi vichanga vya jamii hii kuhusu mila na desturi zao. Utafiti huu umeonyesha kuwa Fasihi Simulizi ya Mwafrika ni hai. Utafiti umegundua kuwa, lugha ni kipengele muhimu katika jamii. Hata hivyo, utafiti umetambua kuwa, wakati mwingine lugha hutumiwa vibaya na wanajamii kumtukuza Mwanamume kupita kiasi na kumpa uwezo na mamlaka dhidi ya mwanamke. Isitoshe, ubabedume umejengwa katika mila, itikadi na utamaduni wa jamii husika. Makala hii imeweka wazi baadhi ya matokeo ya utafiti huu

Upakuaji

Bado hatuna takwimu za upakuaji.
Tarehe ya Uchapishaji
6 Septemba, 2019
Jinsi ya Kunukuu
Kibigo, M., Choge, S., & Simiyu, F. (2019). Tamathali za Semi Zinazosawiri Ubabedume Katika Majigambo ya Miviga ya Shilembe na Mchezasili wa Mayo ya Waisukha, Nchini Kenya kwa Mtazamo wa Semantiki. Jarida La Afrika Mashariki La Masomo Ya Kiswahili, 1(3), 88-97. Retrieved from https://journals.eanso.org/index.php/eajss/article/view/34

Makala zilizo somwa zaidi kama hii.