Utata Katika Ufundishaji wa Isimujamii Katika Shule za Upili Nchini Kenya

  • Martha N Wafula Kibabii University
  • Fred Simiyu Wanjala, PhD Kibabii University
  • Ben Nyongesa, PhD Kibabii University
Sambaza Makala:

Ikisiri

Makala haya yamelenga kubaini utata katika ufundishaji wa kipengele cha isimujamii katika shule za upili Kaunti ndogo ya Teso Kaskazini. Kipengele cha isimujamii kina umuhimu katika lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano na mchango katika ufanisi wa mitihani. Ufundishaji wa isimujamii umekumbwa na malalamishi na lawama kutoka kwa walimu wa Kiswahili. Utafiti huu ulishughulikia lengo moja kuu ambalo ni kubaini chanzo cha utata katika ufundishaji wa isimujamii kwa kurejelea vitabu vya kiada. Malengo mengine ya mada ya utafiti yalikuwa pamoja na kupambanua mifumo ya uwasilishaji wa vipengele vya isimujamii katika vitabu vya kiada na kudadavua mikakati inayotumiwa kuvitathmini vipengele vya isimujamii katika shule za upili. Utafiti huu ulilenga kuvitazama vitabu vya kiada ili kubaini chanzo cha utata katika ufundishaji wa isimujamii.  Mtafiti aliongozwa na nadharia ya uamilifu wa muktadha iliyoasisiwa na Thomas Stitch. Idadi ya walimu kumi na wanane wanaofundisha somo la Kiswahili kutoka shule teule walishirikishwa kwenye utafiti. Data asilia ilikusanywa kwa njia ya uchanganuzi wa matini na mahojiano ya ana kwa ana baina ya mtafiti na watafitiwa. Data ya utafiti ilichanganuliwa kwa mujibu wa malengo makuu ya utafiti kwa kuongozwa na nadharia ya utafiti. Matokeo yaliwasilishwa kwa maelezo na asilimia.  Matokeo yalionyesha kuwa vitabu vya kiada vinachangia utata uliopo katika ufundishaji wa isimujamii katika shule za upili. Hata hivyo utata uliopo unaweza kuondolewa iwapo utakabiliwa ipasavyo. Mtafiti alipendekeza kuwa vitabu vya kiada viangaliwe upya ili kuondoa udhaifu uliopo. Wizara ya elimu na Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala (T. U. M. K) iweze kuidhinisha vitabu maalum vya kutumika kwa ufundishaji wa isimujamii katika shule za upili. Mtaala wowote kabla ya kuanzishwa ufanyiwe majaribio ili kutathmini ubora na udhaifu wa utendakazi wake.

Upakuaji

Bado hatuna takwimu za upakuaji.
Tarehe ya Uchapishaji
22 August, 2019
Jinsi ya Kunukuu
Wafula, M., Wanjala, F., & Nyongesa, B. (2019). Utata Katika Ufundishaji wa Isimujamii Katika Shule za Upili Nchini Kenya. Jarida La Afrika Mashariki La Masomo Ya Kiswahili, 1(2), 42-47. Retrieved from https://journals.eanso.org/index.php/eajss/article/view/24