Jinsi Mtindo Katika Ushairi Unavyofundishwa Katika Shule za Upili: Mfano wa Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini, Kaunti ya Busia, Kenya

  • Hillary Mauka Mukoya Kibabii University
  • Misiko Wasike, PhD Kibabii University
  • Deborah Nanyama Amukowa, PhD Maseno University
  • Edwin Masinde, PhD Kenyatta University
Sambaza Makala:

Ikisiri

Makala hii inahusu jinsi ambavyo mtindo katika ushairi unavyofundishwa katika shule za upili nchini Kenya. Wasomi mbalimbali wametafiti kuhusiana na jinsi ambavyo vipengee tofautitofauti vya ushairi vinavyobainika. Aidha, wasomi hao wametafiti kuhusiana na namna ya kufundisha ushairi. Japo tafiti nyingi zimefanywa kuhusiana na ushairi, pana haja kubwa ya kufanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kufundisha mtindo katika ushairi. Hiki ndicho kichocheo cha makala hii. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya utanzu iliyoasisiwa na Boas na kuendelezwa naye Bakhtin. Nadharia hii ina mihimili kadhaa lakini mhimili unaoshikilia kuwa tanzu huibua muundo wa kazi fulani ya fasihi na kufanya kazi hiyo ieleweke kwa urahisi sana, ndio uliotumika katika utafiti huu. Utafiti huu ulitumia sampuli ya utabakishaji kuteua shule zilizoshiriki utafiti huu. Sampuli ya kimakusudi ilitumiwa kuteua walimu kwa sababu hao ndio walio na mamlaka ya kufundisha. Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini ina shule thelathini (30), hivyo basi utafiti ulizingatia asilimia thelathini (30%) kwa kuteua shule tisa (9). Utafiti huu ulitumia mbinu ya usaili na mbinu ya uchunzaji kukusanya data zilizohitajika. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa walimu walitumia maigizo, maswali na majibu, kazimradi, majadiliano, vikundi vya majadiliano, kanda au santuri, kukariri, kinuruweo na maelezo kama mbinu za ufundishaji kufundishia mtindo katika ushairi. Utafiti huu unapendekeza kuwa walimu wa Kiswahili watilie maanani mbinu mahususi wanapofundisha ushairi ili wanafunzi wachangamkie somo la ushairi. Vilevile, unapendekeza kuwa taasisi zinazokuza mitaala ziweze kuzingatia pakubwa sana mbinu mahususi ambazo zitatumiwa na walimu kwa ajili ya kuboresha zaidi ufundishaji wa ushairi. Aidha, unapendekeza kuwa tafiti nyingine zifanywe kuhusiana na jinsi ya kufundisha vipengee vingine vya ushairi kando na mtindo.

Upakuaji

Bado hatuna takwimu za upakuaji.
Tarehe ya Uchapishaji
30 August, 2019
Jinsi ya Kunukuu
Mukoya, H., Wasike, M., Amukowa, D., & Masinde, E. (2019). Jinsi Mtindo Katika Ushairi Unavyofundishwa Katika Shule za Upili: Mfano wa Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini, Kaunti ya Busia, Kenya. Jarida La Afrika Mashariki La Masomo Ya Kiswahili, 1(3), 80-87. Retrieved from https://journals.eanso.org/index.php/eajss/article/view/32