Ujenzi wa Sifa za Mhusika wa Riwaya ya Kiswahili: Tathmini ya Mchango wa Mandhari katika Kiu na Kidagaa Kimemwozea

  • Wyckliffe Collins Jaoko Chuo Kikuu cha Mount Kenya
  • Stanley Adika Kevogo Chuo Kikuu cha Jaramogi Oginga Odinga cha Sayansi na Teknolojia
Keywords: Mandhari, Uyakinifu, Uhusika, Mhusika
Sambaza Makala:

Ikisiri

Mandhari hufasiliwa kuwa ni wakati na mahali patendekapo kadhia, visa au matukio katika utungo wa kifasihi unaohusika. Mandhari yanaweza kuwa halisi au ya kufikirika. Utafiti ulioichipuza makala hii uliazimia kuchunguza usawiri wa mandhari katika riwaya ya Mohamed S. Mohamed, Kiu pamoja na ile ya Ken Walibora, Kidagaa Kimwemwozea. Ingawa malengo muhsusi ya utafiti yalikuwa matatu, makala hii inazamia lengo moja tu - kutathmini mchango wa mandhari katika ujenzi wa sifa za wahusika katika riwaya ya Kiu na Kidagaa Kimemwozea. Tathmini yenyewe imekitwa kwenye mseto wa nadharia mbili - Uhalisia na Umuundo. Nadharia ya Uhalisia inachimuza uyakinifu wa mandhari ya kijamii ilhali nadharia ya Umuundo ikasisitiza dhima na uhusiano wa vipengele vya sanaa. Utafiti huu wenye mkabala wa kithamano ulifanywa maktabani kwa kuzingatia muundo wa kiuchanganuzi. Eneo la utafiti ni fasihi andishi, hususan utanzu wa riwaya ya Kiswahili. Idadi lengwa ya utafiti ni riwaya 10 za kiuhalisia zinazosawiri mandhari halisi. Sampuli ya riwaya mbili, Kiu na Kidagaa Kimemwozea, iliteuliwa kwa usampulishaji dhaminifu. Riwaya hizi ziliteuliwa kwa misingi ya wingi wa vifani vilivyochunguzwa, yaani usawiri wa mandhari. Pamoja na kuakisi malengo ya utafiti, utunzi wa riwaya teule unaambatana na mihimili ya mseto wa nadharia za utafiti. Data msingi ya utafiti ilikusanywa kwa usomaji wa kina wa matini za riwaya teule. Nazo data za upili zikakusanywa kwa usomaji wa kina wa vitabu, tasnifu na makala anuwai za kitaaluma. Data zilizokusanywa ziliainishwa kwa mujibu wa mihimili ya nadharia na malengo ya utafiti. Zilichanganuliwa kwa mujibu wa yaliyomo na matokeo kuwasilishwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yanadhihirisha kwamba mandhari yana mchango wa moja kwa moja katika ujenzi wa sifa za wahusika. Mandhari hayo ni kama vile: ya mahali(upembeni mwa Mto Kiberenge, chumba cha Mtemi Nasaba Bora, msituni, seli, chumba cha Mzee Mwinyi na mandhari ya mitaa kama wa vibyongoni, Selea, Ukele na mingineyo) na ya kiwakati (enzi za kikoloni,miaka mitano, Vitaa Vikuu vya Pili vya Dunia na kadhalika). Mandhari haya yalisukwa kwa ustadi ambao ulichangia ukuzaji wa sifa za wahusika kwa urahisi mno. Matokeo ya utafiti huu yana tija kwa wanariwaya na wahakiki wa kazi za kifasihi kwa jumla. Yatawasaidia kutunga visa vinavyosawiri na kuakisi mandhari kuntu. Isitoshe, wahakiki wa kazi za fasihi watawezeshwa kubaini na kutathmini mandhari anuwai pamoja na dhima zao katika kazi za kifasihi.

Upakuaji

Bado hatuna takwimu za upakuaji.

Marejeleo

Adam, E. (2014). The comparative grammaticality of the English comparative. (Haijachapishwa): Straford University.

Buliba, F.O. na wenzie. (2014). Relative Effects of Cooperative Learning Approach on Secondary School Students’ Attitude in Kiswahili Language Comprehension in Kisii Central Sub County. International Journal of Humanities, Social Sciences and Education, 4(3), 2349-2381.

Burhan, Z. (1987). Mwisho wa kosa. Nairobi: Longman Publishers.

Kombo, D. na Tromp, D. (2006). Proposal and Thesis Writing. Nairobi: Pauliness Publications.

Massoud, S.R. (2022). Kuchunguza Taswira katika Nyimbo za Taarab za Kimahaba za Khadija Kopa. Tasnifu ya Uzamifu (Haijachapishwa). Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Matei, A. (2012). Fani ya Fasihi Simulizi kwa Shule za Upili. Nairobi: Oxford University Press.

Matei, A. (2017). Chozi la Heri. Nairobi: One Planet Publishing & Media Services.

Mohamed, S. (1972). Kiu. Nairobi: Longman Publishers.

Mwangi, D. (2005). Uhakiki wa Fani katika Tamthilia za K.W. Wamitila. Tasnifu ya Uzamili (Haijachapishwa). Nairobi: Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ntarangwi, M. (2004). Uhakiki wa Kazi za Fasihi. Illinois: Augustana College, Rock Island.

Read, S.J. (1987). Constructing causal scenarios: A knowledge structure approach to causal reasoning. Journal of personality and social psychology, 52(2), 288.

Rief, S. (2012). How to Reach and Teach Children with ADD/ADHD: Practical Techniques, Strategies and Interventions, 2nd edition. San Frasisco: Jossey-Bass Publishers.

Walibora, K. (2012). Kidagaa Kimemwozea. Nairobi: Target Publications.

Wamitila, K. (2002). Uhakiki wa fasihi: Msingi na vipengele vyake. Nairobi: Phoenix Publishers.

Wamitila, K. (2003). Kamusi ya fasihi: Istilahi na nadharia. Nairobi: Focus Books.

Wamitila, K. (2008). Kanzi ya fasihi I: Uchanganuzi wa fasihi. Nairobi: Vide~Muwa Publishers.

Tarehe ya Uchapishaji
7 July, 2025
Jinsi ya Kunukuu
Jaoko, W., & Kevogo, S. (2025). Ujenzi wa Sifa za Mhusika wa Riwaya ya Kiswahili: Tathmini ya Mchango wa Mandhari katika Kiu na Kidagaa Kimemwozea. Jarida La Afrika Mashariki La Masomo Ya Kiswahili, 8(2), 67-81. https://doi.org/10.37284/jammk.8.2.3281